Mchumi wa Halmashauri ya Mji Nanyamba Ndugu Sylivester Ngonyani, Mganga wa Halmashauri ya Mji Daktari Hamis Msangawenga na katibu wa Afya wa Halmashauri ya Mji Ndugu, Neema Shaibu wakiwa katika mafunzo ya matumizi ya mfumo wa PlanRep kwa watendaji wa serikali yaliyofanyika katika ukumbi wa NAF Apartment ulioko mjini Mtwara leo
Mfumo mpya wa kuandaa mipango na bajeti za Mamlaka za Serikali za Mitaa (PlanRep) ulioboreshwa umetajwa kuwa muarobaini wa changamoto nyingi za mfumo wa utoaji wa huduma kwa wananchi. Mfumo huu ambao unatarajiwa kuanza kutumika Oktoba 2017 umekuwa ukifanyiwa majaribio ambayo yameonesha tija.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya matumizi ya mfumo huo kwa watendaji wa serikali yaliyofanyika katika ukumbi wa NAF Apartment ulioko mjini Mtwara leo, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara Elias Nyabusani aliyekuwa akimuwakilisha Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara ALfed Luanda amesema Mfumo huu umekuja kama mkombozi kutokana na kutatua changamoto nyingi ambazo serikali imekuwa ikikutana nazo.
Amesema mfumo huu mpya unawawezesha wananchi kupanga mipango na bajeti kulingana kituo au mtoa huduma husika tofauti na mfumo unaotumika sasa ambao vipaumbele na mipango ya Bajeti inaishia ngazi ya Halmashauri.
Ameitaja changamoto nyingine iliyokuwepo kabla ya matumizi ya mifumo ya kielektolini kuwa serikali ilikuwa inaingia gharama kubwa kugharamia posho za maafisha katika kufuatilia taarifa kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Amesema licha ya kupoteza gharama kubwa pia serikali ilikuwa likipoteza muda na hivyo kupunguza ufanisi wa kazi.
Amesema kupitia mfumo huu mpya suala hilo halitakuwepo na badala yake mwananchi anaweza kutumia kompyuta yake au simu ya mkononi kupata taarifa na kutoa mrejesho kwa haraka zaidi.
Nyabusani amewataka wajumbe kuhakikisha wanatumia fursa hiyo kuonesha utendaji kazi uliotukuka. Pia amewashukuru waandaaji wa mafunzo hayo ambao ni Shirika la maendeleo la watu wa Marekani (USAID) kupitia program yao maalumu ya PS3 ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa karibu zaidi na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za MItaa (TAMISEMI). Amesema yako mambo mengi ambayo yamefanywa na PS3 ambayo watanzania wote wanapawa kushukuru.
Kwa upande wake Mkuu wa timu ya Rasilimali Fedha ya PS3 Gemin Mtei amesema PlanRep iliyoboreshwa inakuja kuboresha uwazi ambapo watoa huduma katika ngazi ya halmashauri au mkoa wataweza kupata mrejesho wa kazi zao kwa urahisi zaidi kutokana na ukweli kuwa mtumiaji amepewa nafasi ya kufungua taarifa katika eneo lolote kwa kutumia Kompyuta au simu ya mkononi.
Mafunzo ya siku Nane ya Mfumo mpya wa kuandaa mipango na bajeti za Mamlaka za Serikali za Mitaa (PlanRep) ulioboreshwa yamefunguliwa katika ukumbi wa NAF apartment yakiwahusisha Maafisa Mipango, Wahasibu, Maafisa TEHAMA, Makatibu wa Afya na Waganga Wakuu kutoka Halmshauri na Mikoa. Mikoa iliyoshiriki katika kituo cha Mtwara ni Mtwara, Ruvuma, Lindi na Dar es Salaam
NANYAMBA, MTWARA.
Sanduku la Barua: P.O.BOX 1490,
Simu: +255
Simu:
Barua pepe: td@nanyambatc.go.tz
Copyright ©2016 Nanyambatc . All rights reserved.