VIDEO WANAWAKE WAKICHEZA KUFURAHIA SIKU YA MWANAMKE KIJIJINI
Halmashauri ya Mji Nanyamba yaadhimisha siku ya mwanamke anayeishi kijijini, maadhimisho yafanyika katika kijiji cha Majengo kata ya Njengwa huku mgeni rasmi akiwa ni diwani wa kata hiyo, Mhe. Moza Kapela.
Afisa maendeleo Halmashauri ya Mji Nanyamba, Bw. Keneth Msanchi aelezea juhudi zinazofanywa na serikali katika kumkomboa kiuchumi na kijamii mwanamke anayeishi kijijini hususani kwa Halmashauri ya Mji Nanyamba, ikiwemo kutoa pembejeo za kilimo bure hasa kwa msimu huu wa korosho. Aliendelea kwa kusema “serikali imetenga Bilioni 84 kwaajili ya mradi wa maji Makonde, utakaonufaisha kata 10 za halamshauri yetu hivyo kumtua ndoo mwanamke aishiye kijijijini, pia imeanzisha majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi kuanzia ngazi ya kijiji.”
Nae mratibu wa Halmashauri ya Mji Nanyamba Dawati la jinsia, Bi. Chipengwa Chisonjela aliwahimiza wanawake kuunda vikundi vya jukwaa la wanawake na kuvisajili vipate kutambulika rasmi ili waweze kunufaika na fursa zitakazojitokeza.
Kwa upande wa afya, Dkt. Shamila Athumani mganga wa kituo cha afya Majengo aliwataka wanawake pindi wapatapo ujauzito kuanza kliniki mara moja pia asisitiza umuhimu wa kujifungulia katika kituo cha afya na kuwataka waache tabia za kuwaomba wazee wao wawazalishe nyumbani.
Aidha, Mhe. Moza aligusia suala la elimu hasa kwa mtoto wa kike na kuitaka jamii kuhakikisha inawapatia haki ya elimu “Ni marufuku kumuozesha mtoto wa kike akiwa mdogo, wakina mama tusimae na kukemea.” Pia aliwataka wanawake kuwa na maamuzi kiuchumi kwani mwanamke ni kiungo kikubwa Kwa familia.
Oktoba 15, kila mwaka Tanzania huadhimisha siku ya kimataifa ya mwanamke anayeishi kijijini ikiwa ni utekelezaji wa Azimio la Umoja wa Mataifa namba 62 lililopitishwa tarehe 18 Disemba 2007 kwa lengo la kutambua jitihada na mchango wa wanawake wanaoishi vijijini kwenye maendeleo ya jamii hususani katika nyanja za uzalishaji wa mazao ya Kilimo na uvuvi. Mwaka 2023 maadhimishi yanabebwa na kauli mbiu ya “Wezesha wanawaje kijijini kwa uhakika wa lishe na uendelevu wa familia.”
NANYAMBA, MTWARA.
Sanduku la Barua: P.O.BOX 1490,
Simu: +255
Simu:
Barua pepe: td@nanyambatc.go.tz
Copyright ©2016 Nanyambatc . All rights reserved.