Waratibu wa TASAF kutoka wilaya ya Mtwara, Halmashauri ya Mji Nanyamba pamoja na kamati za usimamizi ngazi ya jamii (CMC) leo tarehe 10/10/02023 wamefika kwenye kijiji cha Kiwengulo kilichopo kata ya Mnongodi na kijiji cha Nachuma kilichopo kata ya Kiromba kutembelea wanufaika pamoja na kukagua miradi iliyoanzishwa kupitia fedha za ruzuku walizopokea kwa awamu ya kwanza.
Halmashuri ya Mji Nanyamba ni miongoni mwa Halmashauri zinazotekeleza mpango wa kunusuru kaya masikini chini ya TASAF. Mapema mwaka huu TASAF ilitoa ruzuku ya uzalishaji kwa kaya maskini yenye lengo la kuwezesha kaya hizo kuongeza kipato, fursa na uwezo wa kugharamia mahitaji muhimu ya kibinadamu pamoja na huduma za elimu na afya. Kabla ya kupatiwa fedha hizo, TASAF iliwajengea uwezo juu ya namna ya kuzalisha kipato.
“Wote tunajua kuwa korosho ni zao la msimu sasa zile fedha mlizopatiwa na zitakazokuja awamu nyingine tena ni kwaajili ya kutekeleza lile wazo lako la biashara ili uwe na kipato endelevu uondokane na umasikini”. Alisema Bi. Maleso D. Chogo, Afisa ufuatiliaji wilaya ya Mtwara.
Nae Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Mji Nanyamba, Bw. Adamu Matinyi aliwaambia wanufaika hao kuwa haitakuwa busara wajumbe kutoka benki ya dunia wakifika kuwatembelea na kukuta hakuna mabadiliko ya hali zao kichumi. Aliongeza kwa kusema TASAF haitasita kuwachukulia hatua wanufaika walipokea fedha ya ruzuku ya uzalishaji pasipo kuzalisha kitu chochote.
Wanufaika wa TASAF walieleza namna walivyotumia fedha za ruzuku ya uzalishaji kwa kuanzisha miradi mbalimbali ikiwemo ufugaji wa mbuzi na kuku pia kilimo cha mbogamboga, biashara ya mghahawa wa chakula pamoja na kununua mashine kwaajili ya kukodisha wakati wa kipindi cha kupulizia dawa mikorosho. Pia waliiomba serikali kuwapelekea awamu ruzuku awamu ya pili ili waweze kuendeleza miradi yao waliyoianzisha.
NANYAMBA, MTWARA.
Sanduku la Barua: P.O.BOX 1490,
Simu: +255
Simu:
Barua pepe: td@nanyambatc.go.tz
Copyright ©2016 Nanyambatc . All rights reserved.