Na Mhandishi
Jumuiya ya Kimataifa, tarehe 3 Mei 2018 inaadhimisha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani sanjari na Jubilei ya Miaka 25 tangu siku hii ilipoanzishwa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1993. Itakumbukwa kwamba, mwaka huu pia, Umoja wa Mataifa unasherehekea kumbu kumbu ya miaka 70 tangu Tamko la Haki Msingi za Binadamu litolewe.
Hii ni siku ambayo wanahabari hukutana kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali yanayohusu tasnia hii. Ni katika hii siku ndipo wanahabari na wadau wa vyombo vya habari ulimwenguli hupata fursa ya kujumuika pamoja na kujadili kwa kina changamoto zinazowakumba wanahabari katika mazingira yao ya kazi na maisha ya kila siku.
Pichani ni viongozi na wajumbe wa chama cha wanahabari Mtwara wakiwa na Mkurugenzi wa Mji Nanyamba.
Mkoani Mtwara katika kuadhimisha siku hii, Chama cha waandishi wa Habari mkoa wa Mtwara MTPC kimetumia siku hii kufanya shughuli za kijamii kama kusomba mawe kwa ajili ya ujenzi wa bwalo katika shule ya sekondari ya Kutwa Nanyamba, Kushiriki Ufunguzi wa mafunzo kwa watoaji huduma wa vituo vya afya na walimu wa shule za msingi kwa Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipoaumbele (NTD).
Wanahabari wakishiriki zoezi la usombaji mawe katika Ujenzi wa Bwalo, Shule ya Sekondari ya Kutwa Nanyamba
Katika ujenzi wa bwalo, wanahabari kwa umoja wao wakishiriki ipasavyo huku wengine wakionekana kuhamasika zaidi hadi katika ushiriki huo. Mkuu wa Shule, Mwl. Christopher Zahabu akitoa shukrani alisema, “Nitoe shukrani zangu za dhati na pongezi kwa waaandishi wa habari Mkoa Mtwara kwa kazi mlioifanya leo. Hii ni hamasa kubwa kwetu sisi walimu na jamii ya Nanyamba kiujumla kwani imetoa somo kwa wanajamii kwa namna gani wanahabari wanathamini shughuli za kimaendeleo”.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Nanyamba, Mwl. Christopher I. Zahabu (Pichani) akitoa maelezo kwa wanahabari juu ya ujenzi wa bwalo shuleni hapo siku ya maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari ulimwenguni.
Aidha, jopo la wanahabari lilishiriki Ufunguzi wa Mafunzo ya utoaji huduma kwa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele (NTD) kwa Halmashauri ya Mji Nanyamba ambayo ilihusisha watoa huduma wa vituo vya afya pamoja na walimu wa shule za msingi. Mratibu wa NTD, Ndg. Mohamedi Tilika (Muuguzi Msaidizi) aliwaeleza wanahabari kuwa mafunzo hayo ya siku moja yamelenga kuwapa uwezo watoa huduma ili waweze kutoa huduma kwa wananchi ipasavyo ili kufikia malengo yaliyowekwa.
Wanahabari wakiwa na wawezeshaji wa mfunzo sambamba na wawezeshwaji katika picha ya pamoja nje ya jengo la darasa, shule ya sekondari ya kutwa Nanyamba.
Katika maadhimisho hayo, wanahabari wa Mkoa wa Mtwara walipata wasaa wa kukaa pamoja na Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mji wa Nanyamba na kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu habari na jamii. Katika majadiliano hayo ambayo yalitoa fursa kwa wadau mbalimbali wa habari katika baraza hilo kueleza kero yoyote inayohusu tasnia ya habari kwa Nanyamba.
Wanahabari wakiwa katika majadiliano pamoja na wajumbe wa baraza la madiwani la Halmashauri ya Mji wa Nanyamba katika Ukumbi wa Chuo cha Maarifa ya Nyumbani.
Katika kufunga majadiliano hayo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Nanyamba, Wakili Oscar A. Ng'itu aliwashukuru wanahabari na kuwapongeza kwa maamuzi yao kuja kuadhimisha siku muhimu katika Halmashauri ya Mji Nanyamba. Aidha, aliwasihi kuacha tabia ya kufanya mahojiano (Interview) kwa kustukiza bila kumuandaa mhusika kwani imekuwa ikileta shida saana kwa hizi sasa.
Mkurugenzi wa Mji, Wakili Oscar A. Ng'itu akitoa neno kwa wanahabari
NANYAMBA, MTWARA.
Sanduku la Barua: P.O.BOX 1490,
Simu: +255
Simu:
Barua pepe: td@nanyambatc.go.tz
Copyright ©2016 Nanyambatc . All rights reserved.