Watumishi wa Halmashauri ya Mji Nanyamba leo wamefanya zoezi la jogging lililopambwa na shughuli za usafi katika kituo cha mabasi cha Nanyamba. Zoezi hilo limehusisha idara mbalimbali za halmashauri kwa lengo la kujenga afya, mshikamano miongoni mwa watumishi na kuhamasisha jamii kushiriki katika kulinda mazingira.
Mbali na jogging, watumishi hao wameshiriki kusafisha maeneo ya kituo cha mabasi kwa kufagia, kuzoa taka na kusafisha mifereji, hatua ambayo imepokelewa kwa furaha na wananchi waliokuwepo eneo hilo.
Akizungumza baada ya zoezi hilo, kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Nanyamba, Ndg. Walyama Sospeter Tundosa, aliwapongeza watumishi kwa mshikamano na ushirikiano waliouonesha, akibainisha kuwa michezo na usafi ni nyenzo muhimu za kujenga afya bora na mazingira safi. Pia aliahidi kuwa halmashauri itaendelea kuunga mkono shughuli hizo ili ziwe endelevu.
Kwa upande wake, Afisa Utumishi wa Halmashauri, Bi. Susan Michael Ndawi, aliwapongeza watumishi kwa kujitolea kushiriki zoezi hilo na akasisitiza kuwa mshikamano, nidhamu na ushirikiano wa aina hiyo huongeza ufanisi wa kazi na kulijenga vyema taifa.
Wananchi wa Nanyamba nao wametoa pongezi kwa watumishi hao kwa kuonesha mfano wa vitendo katika suala la utunzaji wa mazingira na kuahidi kushirikiana nao mara kwa mara kuhakikisha mji unakuwa safi na wenye mandhari bora.
NANYAMBA, MTWARA.
Sanduku la Barua: P.O.BOX 1490,
Simu: +255
Simu:
Barua pepe: td@nanyambatc.go.tz
Copyright ©2016 Nanyambatc . All rights reserved.