WATUMISHI WA UMMA WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA WELEDI NA NIDHAMU.
Watumishi wa umma Halmashauri ya Mji Nanyamba wametakiwa kufanya kazi kwa weledi na nidhamu katika kutekeleza majukumu yao wanapowahudumia wananchi.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Mji, Advoc. Oscar Ng’itu alipokuwa akifungua mafunzo elekezi ya awali kwa watumishi wapya wa umma walioajiliwa katika Halmashauri ya Mji Nanyamba, mafunzo yalifanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Kutwa Nanyamba Machi 5, 2018.
Mkurugenzi alisema kuwa msingi wa utumishi wa umma umejikita katika uadilifu, hivyo mtumishi wa umma lazima afanye kazi kwa weledi na nidhamu ya hali ya juu. Aliongeza kuwa Utumishi wa umma huendeshwa kwa misingi yake, Ofisi za Umma haziendeshwi kama tunavyoendesha familia zetu, ni ofisi ambayo ina misingi na miongozo huku akiwasisitiza watumishi wakatoe huduma kwa wananchi bila kuwabagua.
Akiongelea umuhimu wa mafunzo elekezi ya awali kwa watumishi wa umma, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji alisema kuwa watumishi wengi wanatoka katika maeneo tofauti yenye mitazamo tofauti hivyo, kuhitaji kufundishwa utaratibu wa kazi katika serikali. “Mafunzo haya ni muhimu sana unapoingia katika utumishi wa umma. Tunatoka katika maeneo tofauti na tamaduni tofauti hivyo, hata tabia zinakuwa tofauti. Mafunzo haya yanalenga kutufundisha namna utumishi wa umma ulivyo na jinsi mtumishi wa umma anavyotakiwa kuonekana na kutenda kazi” alisema Mkurugenzi.
Aliwataka watumishi hao kubadilika baada ya mafunzo kimtazamo na kiutendaji na kuzingatia viwango vya juu katika utumishi wao “Mnatakiwa mjue nafasi zenu mlizonazo. Sasa msiniangushe, Utawala tulionao ni utawala ambao unapenda kero zianze kukatuliwa kuanzia chini. Mimi siku hizi akija mwananchi ofisini kwangu nitaanza kumuuliza kama amepita kwanza kwako ili tupunguze ile kasi ya wananchi kuja Halmashauri. Huko vijijini kuna timu; afisa ugani, daktari, mratibu elimu, mwalimu mkuu, mkuu wa shule; hawa wote wanatakiwa wawajibike kwako. Kuna changamoto mkienda vijijini kila mmoja anapita njia zake mnakosa kushirikiana kiasi kwamba mnakosa kuwa na lugha moja”.
Aidha, Mkurugenzi aliwataka watumishi wakaishi vijijini kama wananchi wanavyoishi bila kuwabagua. “Sisi sote ni watanzania, yawezekana wengine mnatoka familia bora lakini mazingira ya vijijini unatakiwa kuishi kama wananchi wanavyoishi, msiende huko mkawabagua watu. Muende mkawahudumie wananchi kama ambavyo kanuni na taratibu zinavyotuongoza”. Alisema Mkurugenzi.
Katika Mafunzo hayo, watumishi wa umma wapya walielekezwa mambo mbalimbali yahusuyo Utumishi wa Umma yakiwemo Kanuni na Maadili ya Utumishi wa Umma, Haki na wajibu wa mwajiri na mwajiriwa, Mahusiano kazini, Ukusanyaji mapato, Kazi za kamati za Halmashauri za vijiji, uandishi wa mihutasari ya vikao, uendeshaji wa vikao kwa ngazi ya kata na vijiji na mengineyo.
Mafunzo elekezi ya awali kwa watumishi wapya wa umma yameandaliwa na ofisi ya Mkurugenzi wa Mji Nanyamba kupitia Idara na Vitengo yakishirikisha watumishi wapya 48.
NANYAMBA, MTWARA.
Sanduku la Barua: P.O.BOX 1490,
Simu: +255
Simu:
Barua pepe: td@nanyambatc.go.tz
Copyright ©2016 Nanyambatc . All rights reserved.