VIDEO YA SHEREHE ZA UFUNGUZI WA ZAHANATI YA ARUSHACHINI
Wakazi wa kijiji cha Arushachini kata ya Chawi, Halmashauri ya Mji Nanyamba leo wamejawa na furaha baada ya zahanati ya kijiji kuzinduliwa rasmi ikiwa ni hatua ya kuwaondolea adha ya kufuata huduma za matibabu vijiji vya jirani.Zahanati hiyo iliyokamilika kwa 98% na kugharimu milioni 43 za Kitanzania, ilianza kujengwa mwaka 2019 kwa nguvu za wananchi kushirikiana na Halmashauri ya Mji Nanyamba pamoja na wahisani akiwemo Mhe. Abdallah Dadi Chikota mbunge wa jimbo la Nanyamba ambae leo tarehe 30/09/2023 aliizindua kwa kukata utepe.
Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Nanyamba, Dkt. Vincent Kway alisema zahanati hiyo itaweza kuhudumia watu 1504 pamoja na wa maeneo jirani. Akizungumza na wananchi waliojitokeza kwenye uzinduzi huo, Dkt. Vincent aliwaambia kuwa zahanati hiyo ni yao hivyo wana haki ya kufahamu juu ya upatikanaji wa dawa, matumizi ya fedha na chochote kinachotendeka hapo.
Dkt. Elias Matoja, Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Mji Nanyamba alimshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa vifaa vya shilingi milioni 10. Aliendelea kwa kusema “vifaa vya milioni tano vimeshafika, tuna vitanda viwili vya kulaza wagonjwa na kimoja cha kujifungulia wakina mama, tunasubiri vifaa vingine vikishafika wakina mama huduma zote mtapata hapa.”
Akizindua zahanati hiyo Mhe. Chikota aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa watumishi wa afya, na kuwasihi kuelewa kuwa hiyo ni zahanati hivyo itakuwa ikifanya kazi kwa masaa maalumu isipokuwa ikitokea dharura. Pia aliahidi kusaidia kuboresha zahani katika kuifanya ya kisasa iweze kutoa huduma bora.
Naye Diwani wa kata ya Chawi, Mhe. Mwl. Mkoba alimshukuru Mbunge kwa moyo wake wa kujitolea pia aliwasifu wananchi kwa mshikamano katika kuhakikisha zahanati inakamilika.
Zahanati ya Arushachini kwa sasa ina mtoa huduma wa afya mmoja ambapo inatarajia kuajiri watumishi wengine kama ahadi ya waziri wa nchi ofisi ya Rais Tamisemi, Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati wa ziara ya Mhe. Rais aliposimama Nanyamba kusalimia wananchi 16/09/2023.
NANYAMBA, MTWARA.
Sanduku la Barua: P.O.BOX 1490,
Simu: +255
Simu:
Barua pepe: td@nanyambatc.go.tz
Copyright ©2016 Nanyambatc . All rights reserved.